
ANDREY Coutinho, amefurahishwa na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji na viongozi wa Yanga, lakini amekiri kwamba anakiona chamoto uwanjani kutokana na uchakavu wa uwanja wanaofanyia mazoezi wa Bandari, uliopo jijini Dar es Salaam. Amekiri unamkwaza.
Coutinho,alisema amekuwa akishindwa kufanya kwa nguvu zote kile ambacho akili yake inataka mazoezini kutokana na ugumu wa uwanja ambao tayari umeshamtoa ngozi ya juu ya magoti yake.
Mchezaji huyo alisema amefurahishwa na jinsi mashabiki na benchi la ufundi linavyompa sapoti, lakini bado hawajaona kwa vitendo kile alichodhamiria kukifanya, hivyo akasisitiza watulie wampe muda asome ramani na kuzoea mazingira.
Alisema anahitaji muda kuzoea hali hiyo jambo ambalo linaweza kumfanya kushindwa kucheza vizuri kwa muda muafaka. Yanga tangu ianze mazoezi siku nne zilizopita inatumia Uwanja wa Chuo cha Bandari uliopo Temeke nje kidogo ya jiji. Mchezaji huyo ameshachubuka sehemu ya ngozi yake katika magoti yake hali ambayo inamfanya kuwa mwoga kujituma kwa asilimia zote mazoezini.
“Nafurahi kuona kila mchezaji ni rafiki yangu, tunafurahi na kutaniana hasa Tegete (Jerry) ni rafiki mzuri, kuna changamoto ya uwanja niliumia lakini sasa nakaribia kupona ni kiwanja kigumu tofauti sana na kule Brazil,”alisema Coutinho.
“Kule kwetu kuna viwanja vizuri, nahitaji muda,kuzoea hali hiyo, kwa sasa watu wanaweza kuona sijitumi lakini nakuwa na wasiwasi siwezi kurahisisha kuumia nitazoea hali hii taratibu hasa nikianza kucheza mechi ngumu,”alisisitiza mchezaji huyo gumzo la mashabiki wa Yanga kwa sasa.




 
 
 
 

Post a Comment